Kwa Kiswahili
Kuhusu Jarida
Jarida la Taaluma za Kiafrika la Nordic (Nordic Journal of African Studies / NJAS) ni jarida la wazi la taaluma mtambuka linalochapishwa na Mtandao wa Utafiti wa Kiafrika wa Nordic (Nordic Africa Research Network) na linahusishwa na Forum for Africa Studies (Uppsala University). Hili ni jarida ambalo halitozi gharama za uhariri kwa mwandishi au ada kwa wasomaji wa kazi za kiutafiti zinazochapishwa na NJAS.
Taarifa kuhusu bodi ya wahariri (na mawasiliano yao) pamoja na bodi ya ushauri zinapatikana kwenye kiungo cha wavuti https://njas.fi/njas/about/editorialTeam. Wanaohusika na uhariri katika kila kitengo wameorodheshwa mwanzoni.
Taarifa kuhusu upatikanaji wazi wa Jarida pamoja na sera yake ya hakimiliki soma kwenye kiungo cha wavuti https://njas.fi/njas/about kwa lugha ya Kiingereza.
Kutuma Makala
Makala zote zinapaswa kutumwa kupitia njia ya mtandao.
Tunatumia wapitiaji huru wa makala wasiotambuliwa na waandishi ili kuhakikisha kwamba makala zinazochapishwa zina kiwango cha juu cha kimataifa. Mchakato wa uhariri na mtiririko wa uchapishaji wa makala vimeelezewa (kwa Kiingereza) kwenye kiungo cha wavuti https://njas.fi/njas/about/submissions.
Kwa uwasilishaji wa makala zilizoandikwa kwa lugha tofauti na Kiingereza, tafadhali ambatisha ikisiri iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na lugha iliyotumika kuandikia makala. Makala zilizoandikwa kuhusu lugha za Kiafrika, unaweza pia kuongeza ikisiri katika lugha kienzo. Tazama taarifa kuhusu lugha zinazokubaliwa kwenye taarifa ya kila kitengo.
Tafadhali, soma pia sera yetu ya itikeli kwenye kiungo cha wavuti https://njas.fi/njas/ethics kabla ya kutuma makala yako.
Wasiliana nasi kama una swali lolote kuhusu taarifa zilizotajwa hapo juu.
Malengo na Mawanda ya NJAS
Tunapokea makala juu ya tafiti zinazowasilisha maarifa mapya ya kiujarabati na kinadharia katika nyanja za sayansi jamii za Kiafrika, taaluma za historia na kitamaduni, taaluma za lugha za Kiafrika na fasihi ya Kiafrika, pamoja na mapitio ya vitabu. Jarida limegawanyika katika nyanja nne za uhariri:
- Sayansi za jamii ya Kiafrika
- Taaluma za utamaduni na historia ya Kiafrika
- Taaluma za lugha za kiafrika
- Taaluma za fasihi za kiafrika
Makala kuhusu masuala mtambuka pia zinapokelewa na zinashughulikiwa na timu ya wahariri kutoka nyaja husika.
Maelezo juu ya mawanda kwenye nyanja tatu: Sayansi za jamii ya Kiafrika, Taaluma za utamaduni na historia ya Kiafrika pamoja na Taaluma za fasihi ya Kiafrika, yameelezwa kwa lugha ya Kiingereza. Maelezo juu ya mawanda kwenye Taaluma za lugha ya Kiafrika yameelezwa hapa chini kwa lugha ya Kiswahili.
Taaluma za Lugha za Kiafrika
Kitengo cha Taaluma za Lugha kinachapisha makala za lugha na isimu zenye uchambuzi wa kiisimu unaochangia dhana mpya kwenye maswali anuwai kuhusu nadharia za kiisimu zinazoweza pia kuhusisha mada za kiisimujamii. Pia, kitengo kinachapisha makala zinazowasilisha kiwango kikubwa cha data mpya kwenye mada muhimu za lugha ambazo hazijatafitiwa sana. Makala hizo zinaweza kufanya uchambuzi wa lugha bila kuhusisha nadharia za kiisimu ingawaje kwa namna yoyote ile lazima makala hizo ziwe na misingi thabiti kwenye taaluma za isimu na nadharia msingi ya isimu). Vilevile, Kitengo cha Taaluma za Lugha kinachapisha makala kuhusu sera ya lugha; lakini, lazima makala hizo zijikite katika kuwasilisha matokeo ya tafiti zenye mawanda mapana au tafiti ambazo zinatoa mtazamo mpya uliojengewa hoja madhubuti katika mada ya sera ya lugha.
Kitengo cha Taaluma za Lugha kinapokea makala zilizoandikwa kwa Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili.